Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: TAASISI ya Tiba ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) imezindua rasmi mfumo mpya wa kidijitali wa kuweka miadi na madaktari, ujulikanao kama ‘MOI Online Appointment System’, unaolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika hospitalini.
Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika lSeptemba 15, mwakq huu 2025, ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Mpoki Ulisubisya, ambaye amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mfumo huo ni kupunguza usumbufu kwa wagonjwa na kuondoa msongamano wa watu wanaofika hospitalini kwa ajili ya kupanga miadi.

“Kwa kutumia mfumo huu, mgonjwa anaweza kuchagua daktari anayemtaka, tarehe, muda pamoja na kliniki anayoihitaji. Hii itaepusha hali ya kufika hospitali na kukuta daktari hayupo au kliniki haifanyi kazi siku hiyo,” amesema Dkt. Mpoki.
Ameeleza kuwa mara baada ya kuweka miadi, mgonjwa atapokea ujumbe mfupi wa maandishi unaothibitisha miadi yake, Endapo daktari atakuwa na udhuru, taarifa hiyo pia itatumwa kwa mgonjwa kupitia simu yake, kumpa fursa ya kuchagua daktari mwingine au kupanga tarehe mbadala.
Mfumo huo unapatikana saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki, kupitia simu janja, kompyuta mpakato au kishikwambi kwa kutumia tovuti rasmi ya taasisi hiyo: www.moi.ac.tz au moja kwa moja kupitia kiunganishi: https://miadi.moi.ac.tz/appointment/. Mgonjwa atatakiwa kujaza taarifa zake binafsi kabla ya kuwasilisha maombi ya miadi.
“Hii ni hatua muhimu katika utoaji wa huduma bora na kwa wakati. Hata hivyo, wagonjwa ambao hawataweza kutumia mfumo huu hawatanyimwa huduma; wote watapokelewa kama kawaida.
“Tofauti ni kwamba mfumo huu unampa mgonjwa uhakika wa kupata huduma kwa muda anaoutaka na kwa daktari anayemchagua,” amesema Dkt. Mpoki.
Amewahimiza Watanzania kutumia mfumo huo mpya, akisisitiza kuwa ni sehemu ya jitihada za taasisi katika kusogeza huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya kidijitali, sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.