Na Lucy Ngowi
PWANI: KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Hery Mkunda amesema kwamba wamekusudia kuongeza wanachama zaidi ili wawe na sauti kubwa, kwani hivi sasa wapo wamefikia 45,000.
Mkunda ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania ( TUCTA), amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Mfanyakazi Tanzania.
Katibu Mkuu huyo pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika Mashariki, pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Duniani amesema, Tughe mwaka huu imedhamiria inaboresha mafunzo kwa wanachama wake.
“Lakini pia kuhakikisha tunaendelea kuwahudumia wanachama wetu. Huduma kwa wanachama zipo nyingi, moja ni kuwawakilisha wanapokuwa na matatizo mbalimbali kwa waajiri wao.
“Pia kwa kupitia mabaraza ya wafanyakazi kuhakikisha wanapata nafasi ya kushirikishwa vizuri. Kuhakikisha kuna bajeti kwenye mabaraza nako wafanye vikao mara mbili,” amesema.
Ameongeza kuwa, pia kuwapigania kuhusu maslahi yao na kutolea mfano suala la motisha kwa wafanyakazi.
Amesema Tughe imekuwa ikiwakilisha kwenye masuala ya kinidhamu, au mfanyakazi anapopatwa na kesi mbalimbali mahakamani.