Na Lucy Ngowi
DODOMA: MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Profesa Sifuni Mchome, ameipongeza VETA kwa hatua kubwa ya ubunifu katika sekta mbalimbali, huku akitoa rai ya kuingia kwenye uzalishaji mkubwa wa bidhaa hizo ili kukidhi mahitaji ya soko.
Profesa Mchome ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la VETA katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika mkoani Dodoma, ambapo alishuhudia kazi mbalimbali za ubunifu zinazofanywa na wataalamu na wanafunzi kutoka vituo mbalimbali vya VETA nchini.

Katika ziara hiyo, ameona teknolojia mbalimbali zenye ubunifu wa hali ya juu, ikiwemo mashine za umwagiliaji kwa kutumia nishati ya jua, vifaa vya kuchakata chakula cha mifugo kama kuku, na mavazi ya kisasa yaliyotengenezwa na vijana wa VETA.
Amesisitiza kuwa vifaa hivyo vina uwezo wa kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na viwanda iwapo vitaingizwa kwenye uzalishaji kwa wingi.
“Nimefurahishwa sana na kazi inayofanywa na VETA. Hii ni hatua kubwa katika ubunifu wa nishati jadidifu, teknolojia ya kilimo na uzalishaji wa mavazi. Sasa ni wakati muafaka kwa VETA kwenda mbele zaidi na kuanza uzalishaji mkubwa wa vifaa hivi. Soko lipo na lina uhitaji mkubwa,” amesema.

Aidha, ameshauri taasisi hiyo kuandaa mkakati mahsusi wa kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazobuniwa ili zisibaki kuwa maonyesho tu, bali ziwe sehemu ya suluhisho la changamoto za maendeleo vijijini na mijini.
“VETA inaweza kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa. Tukizalisha vifaa hivi kwa kiwango kikubwa, tutakuwa tunasaidia wakulima, wafugaji, na sekta nyingine nyingi,” amesema.
Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu kwa taasisi kama VETA kuonesha mchango wao katika maendeleo ya sekta ya kilimo, ambapo ubunifu na mafunzo ya vitendo yanayoendeshwa na mamlaka hiyo yameendelea kutambuliwa kama kichocheo cha maendeleo ya uchumi wa viwanda.