Na Lucy Ngowi
DODOMA: MWALIMU wa Ufundi wa zana za kilimo ambaye pia ni Mtaalamu wa Kilimo, Gema Tarimo amekua akifundisha utumiaji wa dawa za asili kulinda mimea kwa vijana na wadau wa kilimo.
Gema amesema hayo kwenye Maonesho ya Nanenane ya Kitaifa na Kimataifa yanayoendelea mkoani Dodoma.

Amesema pia anawapa ujuzi vijana wa kuziendesha zana za kilimo, kuzirekebisha na kuchomelea zinapoharibika.
Amesema, ” Kupitia ubunifu wa bustani inayotembea, vijana wanafundishwa jinsi ya kulima hata wakiwa na eneo dogo la nyumbani.
“Bustani hii hutumia vikopo vidogo, viroba, na vifaa vya kawaida vinavyopatikana kirahisi bila kuchafua mazingira,”.
Amesema mbolea ya bustani hutengenezwa kwa kuchanganya uchafu wa vyakula kama nyanya na mboga mboga pamoja na udongo.
” Minyoo huongezwa ili kusaidia katika uundaji wa mbolea, na mimea humwagiliwa maji kidogo yanayochuruzika polepole, hivyo kusaidia uhifadhi wa maji,” amesema.
Amesema Mfumo huo wa kilimo ni wa gharama nafuu, unaotunza mazingira na kuwapatia vijana maarifa ya kujitegemea kupitia kilimo cha miji.