Na Lucy Ngowi
MOROGORO: VITUO vya Utafiti wa Kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dakawa na Ifakara vimeendelea kung’ara kwa mafanikio makubwa katika utafiti na ubunifu wa teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao la mpunga nchini.
Mtafiti na Mratibu wa shughuli za kiutafiti na ubunifu kutoka TARI Dakawa, Dkt. William Suvi amesema kituo hicho, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kimefanikiwa kugundua zaidi ya aina 20 za mbegu bora za mpunga, zinazokidhi mahitaji ya mabadiliko ya tabianchi,
Pia changamoto za kiikolojia katika maeneo mbalimbali ya kilimo nchini.
Ametaja mbegu hizo kuwa ni TXD 306 maarufu kama SARO 5, inayofahamika kwa uwezo mkubwa wa kuzaa.

“Kwa kufuata kanuni bora za kilimo, mkulima anaweza kuvuna hadi tani 7.5 kwa hekta moja sawa na ekari 2.5, Mbegu hii hulimwa kwenye maeneo ya umwagiliaji pamoja na yale yanayohitaji mvua.
“Mbegu nyingine ya kipekee ni TARIRIC3, yenye harufu ya kunukia vizuri, pia inayokoboka vizuri, hivyo kupendwa zaidi na wakulima na walaji.
*Vilevile, mbegu ya TARIRIC2 imebuniwa mahsusi kwa mazingira yenye mvua nyingi na hukomaa mapema ndani ya siku 105 hadi 110.,” amesema.

Amesema TARI imegundua mbegu zinazostahimili mazingira ya udongo wenye chumvi na magadi, ambazo ni
SATO 1 na SATO 9, hufanya vizuri katika mazingira hayo.
Pia, mbegu ya Komboka, inayokomaa kwa muda mfupi, imekuwa mkombozi kwa wakulima wanaohitaji mavuno ya haraka.
Amesema kwenye maeneo ya milimani, yenye ukosefu wa maji ya kutosha, yamepewa suluhisho kupitia mbegu ya NERICA 3 na NERICA 7.
Pia amesema mbali na ugunduzi wa mbegu, TARI imebuni teknolojia ya ‘double row spacing’, ambapo badala ya kupanda mpunga kwa nafasi ya kawaida ya sentimita 20 kwa 20, mpunga hupandwa kwa safu mbili zilizo karibu, hali inayoongeza mavuno kwa asilimia 29.
Amesema teknolojia hiyo ni sehemu ya mapinduzi ya kilimo shadidi, ambayo pia hupunguza matumizi ya rasilimali kama maji na mbolea, huku ikipunguza utoaji wa gesi chafuzi.

Naye Mtafiti kurltoka TARI Ifakara, Abdalah Mpunga amesema wamefanikiwa kuanzisha teknolojia ya kitalu mkeka kilichoboreshwa, ambacho ni mfumo unaowezesha uoteshaji wa miche ya mpunga kwa kutumia eneo dogo.
“Kitalu hiki kinabebeka na kinajikunja kama mkeka, hivyo kinaweza kuandaliwa hata nyumbani kabla ya kuhamishia miche shambani.
“Kitalu hiki kinatumia kilo tatu tu za mbegu kwa eka moja, kwa nafasi ya upandaji ya sentimita 25 kwa 25 kwa kila mche mmoja. Matokeo yake ni miche yenye afya, inayokua kwa haraka na kuleta mavuno mengi kwa mkulima,” amesema Mpunga.
Ametaja kaulimbiu ya teknolojia hiyo kuwa ni ‘Kilimo shadidi: mbegu kidogo, maji kidogo, mavuno mengi’, ikiwa na malengo ya kupunguza migogoro ya kugombea maji na ardhi, pamoja na kulinda mazingira.
Amesema taasisi hiyo inawawezesha wakulima kwa kutumia vifaa vya kisasa kama ‘Leaf Colour Chart’ (LCC), ambavyo vinasaidia kutambua muda sahihi wa kuongeza mbolea ya nitrogen kwa kiasi stahiki, na kutofautisha kati ya magonjwa na upungufu wa madini kwenye mimea.
Kwa ujumla, mafanikio haya ya vituo vya TARI Dakawa na Ifakara yanaonesha dhamira ya dhati ya taasisi hiyo kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanafikia uzalishaji wenye tija na faida zaidi, kupitia sayansi na ubunifu unaoendana na mazingira yao halisi.