Na Lucy Ngowi
MOROGORO: MBEGU bora za miwa zinazozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kibaha mkoani Pwani, zinaendelea kuwa na mchango mkubwa kwa wakulima na viwanda kutokana na uwezo wake wa kutoa tija kubwa, ikiwemo kuvuna hadi tani 200 kwa hekta.
Mtafiti kutoka TARI Kibaha, Msajigwa Mwakyusa, amesema hayo katika maonesho ya nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mkoani Morogoro.

Amesema kuna makundi mawili ya mbegu za miwa zinazotegemea umwagiliaji na zile zinazotegemea mvua.
“Kwa wakulima wa nje, kuna mbegu sita zinazotumika ambazo ni TARSCA 1, TARSCA 2, R570, N47 na nyingine.

“Mbegu hizi zinavumilia ukame, zna tija ya tani 50 hadi 130 kwa hekta, Zinastahimili magonjwa hasa ugonjwa wa fungwe, Zina mikato mingi zaidi ya minne na zina kiasi kikubwa cha sukari,” amesema.
Amesema kwa kutumia mbegu hizo, wakulima wamekuwa wakipata tija mara kwa mara kutokana na uimara wake katika mazingira mbalimbali ya kilimo.
Amesema mbegu zinazotegemea umwagiliaji hulimwa na viwanda, nazo zina uwezo wa kutoa tija kubwa wa tani 80 hadi 200 kwa hekta, zina kiasi kikubwa cha sukari, zinavumilia magonjwa, na zina mikato zaidi ya minne.
Amesema mbegu zote huzalishwa kwa kuzingatia mfumo wa upatikanaji wa mbegu safi na salama, hupitia hatua mbalimbali za matunzo maalum ambazo ni kuchemshwa, kutenganishwa na kukaguliwa.
Amesema zao kuu linalopatikana kwenye miwa ni sukari, hata hivyo, katika mchakato wa uzalishaji wake, hupatikana mazao mengine kama:
molasses hutumika kama chakula cha mifugo, na tafiti zinaendelea kuhusu matumizi yake kama mbolea.
Pia Bagasse (makapi) hutumika katika uzalishaji wa umeme viwandani, briketts mkaa bora hutokana na makapi ya miwa.
Na Filter mud (mabaki) hutumika kama mbolea.
Kwa mujibu wa Mwakyusa, kila sehemu ya muwa ina faida katika mnyororo wa uzalishaji wa viwandani.
TARI Kibaha kama taasisi ya utafiti, inachangia kwa kiasi kikubwa juhudi za kupunguza pengo hilo kwa kuzalisha mbegu bora zenye tija kubwa na zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Mbegu hizo huzalishwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ikiwemo njia ya kifundo ambapo ndani ya wiki sita hadi nane, mbegu tayari huwa imekomaa kwa kupandwa shambani.