Na Lucy Ngowi
ARUSHA: MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imetakiwa kuhakikisha kitufe cha utambuzi wa dereva kinasaidia kudhibiti ajali nchini.
Kitufe hicho cha utambuzi wanapatiwa madereva waliothibitishwa na mamlaka hiyo kwa lengo la kudhibiti ajali.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliiagiza mamlaka hiyo hivi karibuni alipotembelea banda la LATRA, kwenye maonesho ya sehemu ya Mkutano wa 17 wa Mwaka wa Kutathmini Utendaji Kazi wa sekta ya uchukuzi mkoani Arusha.
“Ni muhimu mhakikishe dereva anakitumia kwa usahihi kitufe chake na inapaswa kitufe kiwe kinawatumia taarifa pindi dereva anapoendesha zaidi ya muda unaotakiwa ambao ni saa nane kwa mujibu wa Sheria zilizopo ili mchukue hatua,”amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo amesema mamlaka hiyo inawathibitisha madereva wa vyombo vya moto kibiashara ili kuhakikisha kunakuwa na madereva wenye uweledi na wanaozifahamu Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini.
“Tukiwa na madereva wenye uweledi, nayo itasaidia kupunguza tatizo la ajali, kwa sasa tunawasajili na kuwathibitisha kimtandao kupitia mfumo wa kuwatahini madereva DTS, na wale wanaofaulu tunawapatia vyeti na kitufe cha i-button ambacho wanakitumia mwanzo wa safari mpaka mwisho wa safari yao, na sisi tunafuatilia kwa ukaribu matumizi sahihi ya kifaa hicho,” amesema.
Akielezea changamoto kubwa inayowakabili madereva kwa sasa, amesema ni uchovu, hivyo LATRA inaamini ikipata msukumo wa Serikali wa kuwaagiza madereva wote lazima wathibitishwe na watumie vitufe vya utambuzi, itasaidia katika kudhibiti ajali zinazogharimu nguvu kazi ya Taifa na maisha ya Watanzania kwa jumla.