Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: Makamu wa Rais Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali imeweka kipaumbele cha kimkakati katika kukuza ujuzi, stadi, maarifa na sifa za kuajirika au kujiajiri miongoni mwa vijana na wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu.
Aidha amesema, maendeleo endelevu ya Taifa hayawezekani bila kuwa na rasilimali watu iliyoelimika na yenye uwezo wa kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.
Dkt. Nchimbi amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

Ametoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na vyuo, kuwekeza katika tafiti hususan za sayansi na teknolojia ili kuinua viwango vya tafiti na ubora wa elimu nchini.
Kupitia mpango huo, sekta binafsi inaweza kuchangia maendeleo ya elimu kwa kufadhili tafiti na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko la ajira.
Aidha, Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa Taasisi za elimu na sekta binafsi kuzingatia kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani katika utekelezaji wa mpango huo.

Amesema vyuo na sekta binafsi vishirikiane kubaini ujuzi muhimu unaohitajika sasa na siku zijazo, hususan katika fani za sayansi, teknolojia, ubunifu, tiba, uhandisi na hesabu, ili kuwezesha vijana kushindana na kupata nafasi katika soko la ajira nchini na kimataifa.
Makamu wa Rais pia amesema kwamba ushirikiano baina ya taasisi za elimu na viwanda ni hitaji la lazima katika dunia ya leo, kwani vyuo haviwezi kuwa visiwa vya nadharia pekee, na viwanda haviwezi kukua bila nguvu kazi yenye ujuzi unaoendana na teknolojia na ushindani wa soko.

Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa ya sera na mitaala ya elimu katika ngazi zote, kwa lengo la kuujenga mfumo wa elimu ulio mnyumbufu, jumuishi na unaoendana na vipaji, mwelekeo na mahitaji halisi ya soko la ajira, huku ikizingatia mabadiliko ya teknolojia na ushindani wa kitaifa na kimataifa.
Uzinduzi wa mpango huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Rais aliahidi kuanzisha mpango wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu, kwa lengo la kulinganisha mafunzo na mahitaji halisi ya sekta za kipaumbele za Taifa, ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa kwake.

Mpango wa ushirikiano kati ya taasisi za elimu na viwanda unalenga kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya utoaji wa elimu na utendaji kazi, ili kulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele kama nishati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), na viwanda vya kuongeza thamani.
Aidha, mpango unaweka msingi thabiti wa kujenga kizazi cha wahitimu wenye uwezo wa kuajirika, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa, kwani umeelekezwa kubadilisha mfumo wa elimu ya nadharia kwenda mfumo unaozingatia ujuzi, vitendo, ubunifu na uzalishaji mali.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge, dini pamoja na wadau wa maendeleo, wakiwemo waajiri na wamiliki wa viwanda, wakuu wa taasisi mbalimbali, wakuu wa vyuo pamoja na wanafunzi.








