Na Lucy Ngowi
MBEYA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za matibabu.
Akizungumza leo jijini Mbeya alipotembelea banda la NHIF katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, Waziri Mkuu amesema uwepo wa mfuko huo kwenye maonyesho hayo ni wa msingi kwa kuwa unawafikia vijana wengi.

“Ni muhimu wananchi wakajiunga na NHIF ili wawe na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua. Sekta ya afya ni ya kipaumbele, ndiyo maana Serikali imeweka bima ya afya kwa wote,” amesema.
Aidha, ameutaka mfuko huo kuendeleza jitihada za kutoa elimu na kuhamasisha makundi mbalimbali kama waendesha bodaboda, bajaji, wafanyabiashara na vijana kwa ujumla kujiunga na bima hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa NHIF Mkoa wa Mbeya, Dkt. Eliud Kilimba, amesema lengo la ushiriki wao kwenye maonyesho ni kutoa elimu kwa vijana na wananchi kuhusu faida za kujiunga na mfuko huo.

“Tupo hapa kutoa elimu kuhusu NHIF na kumuwezesha mtu kujiunga moja kwa moja hapa uwanjani. Tunasisitiza umuhimu wa kuwa na bima kabla ya kuugua,” amesema Dkt. Kilimba.
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanaendelea jijini Mbeya, yakilenga kuwajengea vijana uelewa katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.