Na Mwandishi Wetu
BELARUS: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameomba Watanzania wapewe fursa za mafunzo katika Chuo cha Kilimo cha Belarus ili kujenga uwezo wa kitaalamu utakaosaidia kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini.
Akizungumza mara baada ya kutembelea chuo hicho akiwa kwenye ziara rasmi ya siku mbili nchini Belarus, Majaliwa amesema elimu ya kilimo kwa vitendo inayotolewa chuoni hapo ni fursa adhimu kwa Watanzania kupata maarifa ya kisasa yatakayosaidia kuongeza tija na usalama wa chakula nchini.

“Watanzania wakipata elimu bora ya kilimo, wakirudi wataibadilisha nchi yao. Tutaleta mapinduzi ya kijani kwa kutumia teknolojia na ujuzi mpya,” amesema.
Waziri Mkuu amehimiza kuanzishwa kwa ushirikiano kati ya chuo hicho na taasisi za elimu za ndani, huku akiahidi kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.
Mbali na elimu,Majaliwa pia alitembelea viwanda vya kutengeneza matrekta na zana za kisasa za kilimo na kuhamasisha wawekezaji hao kufungua matawi yao nchini Tanzania.

Amesema uwepo wa viwanda hivyo nchini utapunguza gharama kwa wakulima na kuongeza upatikanaji wa zana bora za kilimo.
Katika siku zake mbili nchini Belarus Julai 2 hadi 23, 2025, Waziri Mkuu ametembelea kampuni nane kubwa za mitaji mjini Minsk na kunadi fursa za uwekezaji nchini Tanzania katika sekta kuu nne za kipaumbele: kilimo, afya, madini na ulinzi na usalama.

Kwenye sekta ya Afya, Waziri Mkuu ametembelea kampuni ya Belmedpreparaty, moja ya wazalishaji wakubwa wa dawa na vifaa tiba nchini Belarus, inayozalisha bidhaa zaidi ya 1,700 zinazouzwa ndani na nje ya nchi.
Ametoa wito kwa kampuni hiyo kuwekeza nchini Tanzania kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa dawa zenye ubora na bei nafuu.
Hivyo Kampuni hiyo imekubali kutuma ujumbe wake Tanzania kwa ziara ya tathmini ya uwekezaji.
Akizungumzia sekta ya madini baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza mitambo ya kuchimba migodini, amewahamasisha wawekezaji hao kuja kuwekeza nchini ili kuongeza ufanisi wa uchimbaji na kuchochea ukuaji wa sekta hiyo muhimu.

Pia Majaliwa ametembelea kiwanda cha vifaa vya uokoaji na zima moto na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na kiwanda hicho ili kuondoa changamoto ya uhaba wa vifaa vya maokozi nchini Tanzania.
Ziara ya Waziri Mkuu nchini Belarus ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuvutia uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.
