Na Lucy Lyatuu
WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA), umesema magonjwa kazi ikiwemo misuli, mgongo , viuno na shingo yamekuwa yakiongezeka kutokana na kutozingatiwa kwa usalama na afya maeneo mbalimbali ya kazi.
Aidha, umesema kuwa wastaafu walio wengi wanapata magonjwa kazi kutokana na mtindo wa maisha wanapokuwa kazini.
Hayo yamesemwa leo Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Hadija Mwenda alipokuwa akifungua semina ya wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (JOWUTA) .
Amesema kuwa hakuna mazingira ya kazi yasiyo na vihatarishi hivyo, ni lazima Wakala huo kufanya kaguzi za mara kwa mara za afya na usalama ili kuwalinda wafanyakazi wawe na afya njema.
Ameeleza kuwa ajali maeneo ya kazi zimepungua kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na matumizi ya ajili mnemba.
“Tunatakiwa kuweka mifumo dhidi ya vihatarishi vinavyotokea mahali pa kazi. Mtindo wa ukaaji , viti vinavyotumika vinapaswa kuzingatia usalama na afya vinginevyo kuna athari kubwa kiuchumi,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa kutozingatiwa kwa kanuni za usalama na afya huwafanya wafanyakazi kutumia muda mwingi hospitali na kufanya kazi kwa muda mchache na kuishia masikini.
Mwenda amesema kuwa kuna athari kubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa na kwamba sheria hiyo huleta utulivu na kukuza uchumi hivyo, wanaendelea kuwekeza katika kutoa elimu.
Vilevile amesema tathmini waliyoifanya walibaini kuwa bado watanzania Wana uelewa mdogo kuhusu sheria zao, hivyo kwa kutumia waandishi wa habari wanaamini watafikia watu wengi.
Kwa upande wake, Wakili wa OSHA, Rehema Msekwa amesema kila mwajiri katika taasisi, kampuni na viwanda anapaswa kujisajili kwani kwa kukaa kimya wanafanya makosa.
Amesema wafanyakazi wanahaki ya kufanyiwa vipimo na madaktari ambao wamepewa jukumu hilo na OSHA ili kubaini changamoto zao na kuwapangia maeneo sahihi ya kufanyia kazi
Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuwekewa mazingira bora kwa kufuata sheria ya usalama na afya mahali pa kazi.
Amewema kwa ujumla ofisi zote za waandishi wa habari hazina sera ya usalama na afya mahali pa kazi, hivyo waajiri wanapaswa kuzingatia ili wafanyakazi wao waweze kuwa salama.