Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Maji kwa kushirikiana na taasisi binafsi imeandaa mafunzo ya usalama wa mabwawa yatakayolenga kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kuwa salama kwa matumizi yaliyokusudiwa hapa nchini.
Akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Maji, Mtumba jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Robert Sunday, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, alisema mafunzo hayo yatafanyika jijini Mwanza kuanzia Oktoba 21 hadi 23, 2026.
Alitaja taasisi zinazoshirikiana na Wizara hiyo kuwa ni Chemba ya Migodi Tanzania (CMT) pamoja na Kampuni ya Uhandisi ya City, akibainisha kuwa ushirikiano huo unalenga kuimarisha uelewa wa kitaalamu kuhusu usalama wa mabwawa.
Sunday ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wadau na wataalamu wa mabwawa ili kuhakikisha usanifu, ujenzi na uendelezaji wa mabwawa ya maji pamoja na mabwawa ya tope sumu unazingatia viwango vinavyotakiwa.
Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
Washiriki wanaotarajiwa kushiriki ni kutoka serikalini na sekta binafsi, wakiwemo wamiliki wa mabwawa makubwa, wataalamu waliosajiliwa wa mabwawa pamoja na wale wanaohusika na usimamizi wa mabwawa ya maji na tope sumu.
Mafunzo hayo yataongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Usalama wa miundombinu ya mabwawa kuanzia hatua ya usanifu, utumiaji hadi ufungaji.’
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwaalika watunga sera, wataalamu, taasisi mbalimbali na watu binafsi wanaojishughulisha na mabwawa kujisajili kushiriki mafunzo hayo ili kuongeza ufanisi na usalama wa miundombinu hiyo muhimu.

