Na Lucy Lyatuu
MABASI mapya yaendayo haraka ya kampuni ya Mofat yameonekana asubuhi ya leo (2 Oktoba 2025) yakihudumia abiria katika vituo vya mwendokasi kuanzia Gerezani kuelekea Kimara–Mbezi na Kivukoni.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kutembelea kituo cha mwendokasi cha Kimara na kushuhudia changamoto kubwa za usafiri zinazowakabili wananchi.
Chalamila aliahidi kuongeza idadi ya mabasi ili kupunguza msongamano wa abiria unaoshuhudiwa kila siku katika jiji hilo.
Hata hivyo, hali ya usafiri Dar es Salaam imeendelea kuwa na sintofahamu. Jana usiku, majira ya saa mbili, mabasi ya mwendokasi pamoja na baadhi ya vituo ikiwemo Gerezani, Magomeni Mapipa, Magomeni Usalama na Magomeni Kagera vilishambuliwa kwa mawe.
Aidha sababu za mashambulizi hayo bado hazijabainishwa bayana na mamlaka husika.

Awali, magari hayo mapya ya Kampuni ya Mofat yalitarajiwa kuanza kutoa huduma katika njia ya Mbagala. Lakini leo, yameanza kutumika kwenye barabara kuu ya Kimara, Gerezani.