Na Lucy Ngowi
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka ameitaka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuongeza kasi ya kufanya tafiti za aina nyingine za Chanjo za Mifugo ambazo hazijaanza kuzalishwa ili kukidhi mahitaji ya wafugaji nchini.
Dkt. Kusiluka ameyasema hayo alipotemblea banda la TVLA akiambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe lililopo kwenye banda jumuishi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane).
“Nimefurahishwa na kazi mnayoifanya kama Wakala, endeleeni kufanya tafiti za Chanjo nyingine za magonjwa ya Mifugo ambazo hamjaanza kuzalisha ili kukinga Mifugo na magonjwa ambayo yana athari kubwa kwenye ustawi wa Mifugo nchini,” amesema.
Akitoa maelezo kuhusiana na uzalishaji wa chanjo zinazozalishwa na TVLA, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe alisema kuwa TVLA ndio Taasisi pekee ya Serikali inayozalisha chanjo za Mifugo nchini.

Wizara imeomba fedha kwa ajili ya kuendesha kampeni ya uchanjaji mifugo nchini, Chanjo za TVLA ndio zitakazotumika kwenye zoezi hilo muhimu. Chanjo ambazo hazizalishwi na TVLA zitaagizwa kutoka kwa wazalishaji wengine,” amesema.
Aina saba za chanjo zinazozalishwa na TVLA ni pamoja na Chanjo ya Kideri au Mdondo kwa kuku (TEMEVAC), Chanjo ya Homa ya Mapafu ya Ng’ombe (CBPP), Chanjo ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi (CCPP), Chanjo ya Kimeta (Anthrax), Chanjo ya Chambavu (Blackquarter), Chanjo ya Kimeta na Chambavu (Tecoblax) na Chanjo ya Kutupa Mimba (Brucellosis).
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka amepata maelezo kuhusina na huduma mbalimbali zinazotolewa na TVLA zikiwemo uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya Mifugo, Uzalishaji na Usambazaji wa Chanjo za Mifugo, Uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo, Usajili na uhakiki wa ubora wa Viuatilifu vya Mifugo, utafiti wa magonjwa ya Wanyama pamoja na huduma ya ushauri na Mafunzo.