Lucy Lyatuu
PWANI: SERIKALI imesema kongani ya viwanda ya SINO TAN iliyopo eneo la Kwala.mkoa wa Pwani inatarajiwa kujenga viwanda mbalimbali vipatavyo 600 na kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 100,000.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo amesema hayo alipotembelea eneo hilo, na kuahidi kukutana na Shirika la Reli Tanzania ( TRC) ili kuona uwezekano wa kujenga kituo Cha reli katika eneo hilo ili kuharakisha usafiri.
Amesema atahakikisha kusukuma uwekezaji nchini ili kuongeza ajira na kuhamasisha mkoa wa Pwani ambao una uwekezaji mkubwa wa viwanda kuendelea kuongeza uwekezaji.
Amesema katika kongani hiyo uwekezaji mkubwa umefanyika na ameridhika sana na kasi hiyo na kwamba suala la kuongezwa umeme wa MG 50 litafanyiwa kazi kwani lengo ni vifanye kazi Kwa kasi ,vizalishe na kupunguza kutegemea kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kongani hiyo, Janson Huang amesema anashukuru serikali ya Tanzania Kwa ushirikiano mkubwa wa Uendelezwaji wa eneo hilo ambalo Lina ekari zaidi ya 2000.ikiwa ni kubwa zaidi Kwa eneo ambalo limewahi kusajiliwa Kusini mwa Afrika.
Amesema wamekamilisha sehemu ya ujenzi wa viwanda hivyo ambapo zaidi ya viwanda 200 ni viwanda vikubwa na 300 vikiwa ni viwanda vya kati na vidogo.
“Serikali inatoa ushirikiano mkubwa katika eneo hili na tunajua baadhi ya changamoto kama ya umeme,kituo cha reli na kupewa punguzo la Kodi tayari serikali imesikia na itafanyia kazi,” amesema na kuongeza kuwa watafanya kazi Ili kuhamasisha wawekezaji wengi waje nchini.
Awali Waziri Jaffo akiwa katika kongani ya kisasa ya viwanda ( KAMAKA), iliyoko eneo la Mlandizi amepongeza uwekezaji wa wazawa katika eneo hilo lenye ukubwa wa ekari zaidi 1077.
Amepongeza miundombinu ya eneo hilo kuwa iko tayari na viwanda zaidi ya 200 vinajengwa eneo hilo na kwamba atahakikisha masuala ya msingi yanapatikana Ili vijana wengi waweze kupata ajira.
Hata hivyo ameagiza maofisa wa Viwanda, kutoka Wizara yake kumuandikiabtaarifa maalum ya eneo hilo pamoja na changamoto zilizopo Ili zifanyiwe kazi.