Na Danson Kaijage
Migogoro ya ardhi imeendelea kuwa changamoto kubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma, hasa katika Jimbo la Dodoma Mjini. Wananchi wamekuwa wakilalamikia vitendo vya uvamizi, ukosefu wa hati halali za umiliki, pamoja na madai ya mashamba kunyang’anywa bila fidia.
Suala hilo pia limekuwa kikwazo kwa mgombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samwel Kisaro, ambaye amejikuta akilazimika kujibu maswali magumu kutoka kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho.

Wajumbe hao wanadai Kisaro anamiliki kampuni inayojihusisha na upimaji, ununuzi na uuzaji wa ardhi, jambo linaloibua hofu ya mgongano wa maslahi endapo atachaguliwa kuwa mbunge.
“Ndugu mgombea, unatafuta ridhaa ya kuwa mbunge wa Dodoma Mjini, lakini tunakabiliwa na migogoro mingi ya ardhi. Inasemekana una kampuni ya upimaji, je, tukikuchagua utatusaidiaje kupata ardhi yetu bila kuingilia kwa maslahi binafsi?” alihoji mmoja wa wajumbe kutoka Kata ya Ntyuka.
Mjumbe mwingine, Anna Mputa, aliongeza kuwa kuna mashamba yaliyotwaliwa kinyume cha sheria na kutolewa kwa watu wenye uwezo kifedha, huku wamiliki halali wakiachwa bila fidia yoyote.
Akijibu tuhuma hizo, Kisaro amekanusha kumiliki kampuni ya upimaji wa ardhi, japokuwa alithibitisha kuwa anamiliki kampuni nyingine isiyohusiana na shughuli za upimaji.
Ameahidi kushughulikia tatizo hilo kwa kupendekeza mabadiliko ya sheria za ardhi ili kulinda haki za wananchi.
“Nikipewa ridhaa ya kuwa mbunge, nitahakikisha wale wote waliodhulumiwa ardhi yao wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria. Tutapitia upya sheria za ardhi kuhakikisha kila mmoja ananufaika kwa haki,” amesema.
Katika hatua nyingine, mgombea mwenzake kupitia CCM, Robert Mwinje, ametumia jukwaa hilo kuwasilisha ajenda yake kwa wajumbe wa chama, akiahidi kushughulikia matatizo ya ardhi, miundombinu na mgawanyo wa ardhi kwa haki.
Akizungumza katika mkutano wa CCM Kata ya Ntyuka, Mwinje amesema amekuwa akihudumu ndani ya chama kwa muda mrefu kama Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Dodoma, hivyo anauelewa vizuri mkoa huo na changamoto zinazowakabili wananchi.
Licha ya kuachishwa nafasi hiyo kwa tuhuma ambazo hakuzifafanua, Mwinje ameeleza kuwa bado ana dhamira safi na uwezo wa kulitumikia jimbo hilo kwa ufanisi.
Ametaja vipaumbele vyake kuwa ni
kutatua migogoro ya ardhi kwa kushirikiana na taasisi husika,
Kuboresha miundombinu ya barabara ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi.
Vile vile kuweka mfumo thabiti wa mgawanyo na umiliki wa ardhi ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara.
Amekiri changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi na zinahitaji mbunge mwenye uelewa wa ndani ya jamii na dhamira ya kweli.