Na Mwandishi Wetu
KIGOMA: “NAWAPONGEZA Mwenyekiti wa Halmashauri, Makamu wake, Mbunge wa Kasulu Vijijini, madiwani wote, Mkurugenzi na wataalamu kwa kazi nzuri iliyowezesha halmashauri kupata hati safi katika ukaguzi wa CAG kwa mwaka ulioishia Juni 2024. Hongereni sana,”.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina ametoa pongezi hizo wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani kupitia na kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uliofanyika katika Ukumbi wa Kagoma, makao makuu ya halmashauri.

Ngayalina amesema halmashauri hiyo, imepata hati safi na kupunguza idadi kubwa ya hoja hadi kufikia tarakimu moja kwa kuwa na hoja tisa kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Amesema hiyo ni mara ya nne mfululizo, mafanikio ambayo yameipa heshima si tu halmashauri hiyo, bali pia mkoa mzima wa Kigoma.

Pia amesisitiza umuhimu wa kufunga hoja zote zilizosalia kwa vielelezo na kutekeleza maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Amesema lengo la mkoa ni kuhakikisha hoja zote zinapungua hadi kufikia tarakimu moja ifikapo mwaka wa fedha 2025/2026.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Eliya Kagoma,amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya madiwani, wataalamu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, vyombo vya ulinzi na usalama, Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.


Mkaguzi Mkuu wa Nje kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Honest Muya, ameitaka halmashauri hiyo kushughulikia changamoto ya watoto kushindwa kusoma.
Ameahidi ofisi yake kuendelea kutoa ushauri elekezi kuhusu namna bora ya kushughulikia tatizo hilo katika mwaka wa ukaguzi unaofuata.