Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994.
Pamoja na miaka 50 ya utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kupitia taasisi mbalimbaliza serikali nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema hayo leo Machi 5. 2025 alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho hayo ambayo kilele chake kitaadhimishwa kwa siku nne kuanzia Machi 18 hadi 21, Katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Mkoani Dar es Salaam.
Profesa Mkenda amesema katika maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo kutoa huduma kwa jamii zinazoendana na shughuli za ufundi na ufundi stadi ikiwem kupaka rangi majengo ya umma kama Hospitali na Zahanati.
“Pia kukarabati majengo ya shule, kuonesha maonesho ya ubunifu wa teknolojia, kuendesha mashindano ya ujuzi, kutoa tuzo na vyeti vya heshima kwa watu mbalimbali kwa mchango wao katika shughuli za maendeleo ya mafunzo ya ufundi na ufundi stadi nchini,” amesema.