Na Danson Kaijage
DODOMA: HUDUMA ya Kanisa la Gospel Christ Church (GCC) Tanzania, limeanzisha maombi maalumu kwa ajili ya kuliombea Taifa pamoja na kuombea uchaguzi mkuu wa Madiwani,wabunge na Rais.
Maombi hayo yataanza Kesho Februari 21, 2025 eneo la Mbondole Ilala Jijini Dar es Salaam.
Askofu Mkuu wa kanisa hilo Dkt.Daudi Chidawali amesema maombi hayo ni kuhakikisha Taifa linaombewa na linakuwa na utulivu.
Chidawali ameeleza kwa sasa taifa linajiandaa kuingia katika uchaguzi mkuu hivyo ni wajibu wa kanisa kufanya maombi ili kuhakikisha wanapatikana watu ambao wana nia njema ya kuwasaidia watanzania na kutokuwa na ubinafsi.
Amesema maombi ni muhimu kwani ni agizo la Mungu na maandiko yanaeleza wazi kuwa haki uliinua Taifa na haki haiwezi kupatikana kama hayajafanyika maombi ya kuwapata viongozi wenye hofu ya Mungu.
“Tunatakiwa kuelewa kuwa ili kuwa na nchi yenye utulivu ni lazima kuwa na viongozi wacha Mungu na wenye hofu ya Mungu,tunatakiwa kuwachagua watu ambao ni mapenzi ya Mungu kuwa viongozi na siyo kuwa viongozi kwa sababu ya rushwa au vitisho.
“Tunatambua kuwa nchi yetu ambayo inaongozwa na Rais Samia Suluhu Hasani imefanya mambo mengi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka minne hivyo tunapoelekea kwenye uchaguzi tunahitaji kupata viongozi ambao wanatambua juhudi zinazofanywa na viongozi na wakati mwingine kuziendeleza.
“Na hilo litatokana na maombi ya watakatifu,hatuwezi kuwaacha wanasiasa wapambane wenyewe kupinga rushwa au dhuluma kinachotakiwa ni nguvu ya Mungu pekee kufanya kazi na hayo yote yanapatikana kwa maombi tu,” amesema.