Na Danson Kaijage
WIZARA Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo imeeleza mafanikio lukuki katika wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minn ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassani kwa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya michezo.
Palamagamba Kabudi akiwa anazungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa habari -Maelezo Jijini Dodoma amesema mafanikio hayo kwa kipindi cha miaka minne hayajawahi kutokea tangu kupata uhuru.
Ameyataja mafanikio mengine ni pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Mafanikio mengine ni kufuzu kwa Timu za Taifa kwenye mashindano ya Kimataifa, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo kwa ajili ya Mashindano ya AFCON 2027 kwa gharama ya Sh. Bilioni 161.977.
Amesema hatua ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo (BMT), Kuandaa Matamasha matatu ya Kitaifa ya Utamaduni, Mafanikio ya Siku ya Maadhimisho ya Kiswahili, Kufungua Fursa za Lugha ya Kiswahili duniani kote na kufungua Vituo vya Kufundisha Kiswahili Nje ya Nchi ni mafanikio makubwa.
Pia amezungumzia utoaji wa Mikopo kwa wadau wa Sanaa na Utamaduni, Ugawaji wa Mirabaha kwa Wasanii, Uhuishaji na Uendelezaji wa Tamasha la Serengeti Music Festival, Uanzishwaji wa Tuzo za Kitaifa za Ucheshi na Uendelezaji wa Tamasha la Tuzo za Filamu nchini.
“Wizara imefanikiwa Kuimarisha Ukusanyaji Mapato ya kazi za Sanaa, Kuanzisha Mradi mkubwa wa Ujenzi wa Sports and Arts Arena, Mradi wa Jumba Changamani la Filamu na kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari nchini,”amesema kabudi.