Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Maliasili na Utalii imeendelea kutekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyotoka na maoni ya Tume ya Haki Jinai ya kuboresha Jeshi la Uhifadhi kwa kutoa mafunzo ili liweze kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki za binadamu.
Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba ametoa mafunzo hayo kwa askari kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wa mikoa ya Simiyu na Mara.
Amewaeleza askari hao kwamba Taifa lina imani kubwa nao katika ulinzi na usimamizi wa maliasili nchini, hivyo ni vyema wakaitunza tunu hiyo ambayo imetokana na imani ya wananchi kwao.
Aidha, Wakulyamba amewataka askari hao kujiepusha na vitendo viovu kazini, hususan rushwa na kuwabambikia wananchi matukio ya uongo, huku akiwashauri kujenga mahusiano mazuri miongoni mwao pamoja na jamii inayowazunguka..
Ameongeza kuwa katika kuimarisha Jeshi la Uhifadhi hapa nchini, Wizara inaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, likiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi ili kulijengea uwezo wa kiutendaji.
“Tumeanza kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwafundisha askari wetu juu ya kuzingatia kanuni za Haki Jinai katika kutekeleza majukumu yao. Kanuni hizo ni pamoja na ukamataji salama, kuheshimu utu wa binadamu, sheria za upekuzi na kuhodhi mali za uhalifu kisheria,: alisema Wakulyamba na kuongeza.
“Ikiwa ni sehemu ya maoni ya Tume ya Haki Jinai, Jeshi la Uhifadhi litaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwa linauzoefu katika masuala ya utendaji kazi ikiwemo upelelezi na kudhibiti ghasia za kijamii kwa mbinu salama zenye kuzingatia misingi ya haki za binadamu, hivyo utaalam wake na uzoefu ni muhimu kwa ustawi wa sekta ya Maliasili na Utalii,”.
Kadhalika amewaagiza maofisa wa Jeshi hilo kusimamia vyema nidhamu na uadilifu kwa askari wa Jeshi hilo, kwani madhara yanayotokana na utendaji mbovu wa baadhi ya askari hayatakuwa na athari tu kwa maisha yao na familia zao, bali pia yataathiri sifa njema ya taasisi na Taifa kwa ujumla.
Mbali ya kutoa mafunzo kwa askari hao, ametembelea na kukagua shughuli za uhifadhi katika mapori ya akiba ya Ikorongo/Grumet chini ya TAWA, na hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo chini ya TANAPA.
ReplyForward |