Na Lucy Lyatuu
Dar es Salaam: JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema kuelekea mchezo wa soka wa watani wa jadi baina ya klabu ya Yanga na Simba limejipanga kuchukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo huo.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi, Muliro Jumanne amesema hayo jana Dar es Salaam na kuongeza kuwa kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam kutakuwa na mchezo huo wa soka wa watani wa jadi baina ya klabu ya Yanga na Simba utaanzia saa 1:00 jioni.
Amesema usalama utaimarishwa kwa kiwango cha juu na kwamba Jeshi linawakumbusha kuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kwenda na silaha uwanjani isipokuwa vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo.
Kamanda Muliro amesema watu watakaojihusisha na vitendo vya kihalifu ndani au nje ya uwanja watashughulikiwa haraka kwa mujibu wa sheria.