Na Danson Kaijage
DODOMA: WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Seleman Jaffo amewaagiza wanaomiliki viwanda ambavyo vilikuwa mali ya Serikali, vikafa kuhakikisha wanavifufua kabla ya kulazimishwa na Serikali.
Jaffo ametoa agizo hilo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari alipotoa taarifa ya maendeleo ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dodoma.
Amesema Serikali imeelekeza kufufua viwanda vyote ambavyo vilibinafsishwa na kutelekezwa na wamiliki wa viwanda hivyo.
“Nichukue nafasi hii kuwaeleza wamiliki wote ambao walibinafsishwa viwanda na kushindwa kuviendeleza sasa ni wakati wa kuviendeleza kabla ya Serikali haijafuatilia,” amesema.
Pia amesema kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, Wizara ya Viwanda na Biashara imepiga hatua kwa kukuza viwanda vidogo na vikubwa sambamba na kuanzisha uzalishaji wa vifaa vya ujenzi kama vile kiwanda cha nondo,mabati na malumalu.
Amesema katika kukuza na kuboresha viwanda hivyo vimezalisha bidhaa bora, vimeongeza ajira kwa vijana wa kitanzania huku bidhaa hizo zikiuzwa nje ya nchi na Afrika ya kati.
Akielezea mafanikio amesema Serikali imeweza kujenga viwanda vya kutengeneza kioo ambacho kwa sasa kinauzwa ndani na nje ya nchi huku ikiongeza pato la taifa.
Katika hatua nyingine amezungumzia uwepo wa kiwanda cha kutengeneza magari ya kisasa na yenye mwonekano mzuri ambayo yanazalishwa nchini huku akieleza kuwa vipo viwanda ambavyo vinazalisha chuma ambacho kitasaidia kutumika kwenye matengenezo ya magari hayo.
Akizungumzia kiwanda cha General Tyre kilichopo Arusha ambacho hakifanyi kazi kwa takrikabi miaka 20 sasa amesema Serikali iko kwenye mazungumzo na wawekezaj.
Uzalishaji wa matairi ulisitishwa mwaka 2007 kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na teknolojia ya zamani, ukosefu wa mtaji, na ushindani kutoka kwa matairi ya bei nafuu yaliyoagizwa kutoka nje ya nchi, hasa kutoka China.