Na Danson Kaijage
DODOMA: WAZIRI ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Stergomena Tax amesema wamehakikisha tunu za Taifa yaani amani, ulinzi na usalama zinalindwa kwa kuimarisha umoja, mshikamano na utulivu nchini
Amesema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya wizara hiyo kwa Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dodoma.

Amesema pia wizara hiyo imeendelea kuliimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuliongezea bajeti, hivyo kuongeza uwezo wa kimedani kwa kulipatia vifaa, zana za kisasa na kuwezesha mafunzo na mazoezi.
Vile vile serikali imeweza kugharamia ujenzi na uboreshaji wa miundo mbinu mbalimbali, kwa sasa, wizara inaendelea kukamilisha ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa – MMUT (Kikombo-Dodoma) unaogharamiwa na Serikali na kutekelezwa na wataalam wa ndani ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 93.5.
“Aidha JWTZ imeendelea na ujenzi wa Hospitali kuu ya Kanda Dodoma yenye hadhi ya Daraja la nne inayojengwa katika eneo la Msalato katika Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani, Ujenzi wa Hosteli za Chuo cha Taifa cha Ulinzi (Kunduchi, Dar es Salaam),
“Kujenga makazi ya wakufunzi na waalimu waelekezi wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti, mkoani Arusha, ujenzi wa kapera Hospitali Kuu ya Jeshi – Mwanza na Chuo cha TMA – Arusha na ujenzi wa Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Akiba mkoani Singida,” amesema
Mafanikio mengine hali ya ulinzi na usalama wa mipaka kuwa salama.
“Wizara kupitia JWTZ, imeendelea kulinda Amani, kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi yetu, ipo salama.
“JWTZ kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Usalama linaendelea kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vyote vyenye viashiria vya uvunjifu wa amani, na Taifa letu ni salama na lenye utulivu na amani,” amesema
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuwapa vijana wa kitanzania mafunzo ya awali ya kijeshi na stadi za kazi, kuendeleza tafiti na uwahulishaji wa Teknolojia.