Na Lucy Ngowi
GEITA: MBUNGE mstaafu anayegombea tena kiti cha Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Musukuma, amesema kuwa kampuni ya uchimbaji madini ya Fema Mining & Drilling ni mfano mzuri wa kuigwa.
Musukuma amesema hayo alipotembelea banda la Fema katika maonesho ya nane ya madini yanayoendelea mkoani Geita.

“Fema ni Watanzania, wanachimba kwenye mgodi wa Buckreef . Walianza kama kiwanja cha Mpira, mwaka uliofuata wakajenga jengo la utawala. Sasa tunaendelea kusonga mbele na watu,” amesema Musukuma.
Amesema Fema Mining & Drilling ni kampuni ya Kitanzania inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania. Inafanya shughuli zake za uchimbaji, ulipuaji, na uchorongaji katika mgodi wa Buckreef.

Ofisa Usalama wa kampuni hiyo, Victor Mkono amesema Fema imejidhatiti kusaidia jamii inayowazunguka katika nyanja mbalimbali.
Miongoni mwa michango hiyo ni pamoja na kuchimba visima vya maji safi na salama, kuchangia kuendeleza miradi ya shule, kusaidia vifaa vya hospitali, na kushiriki maonyesho mara kwa mara.
Aidha, halmashauri inanufaika na mapato ya Uwajibikaji wa Makampuni kutoka Fema Mining & Drilling kati ya shilingi milioni 159 hadi 400.