Na Lucy Lyatuu, Dodoma
MRADI wa FISH4ACP unaotekelezwa na Shirika La Kilimo La Umoja Wa Mataifa (FAO) umewezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa uvuvi, wakiwemo wavuvi, wachakataji, wasafirishaji na wauzaji wa mazao ya uvuvi, kutumia teknolojia bora za kuboresha uzalishaji wa mazao ya uvuvi.
Aidha matumizi ya teknolojia hizo yamewezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa cha upotevu wa mazao ya uvuvi nchini, kupitia mafunzo ya uchakataji, matumizi ya teknolojia za kukaushia na kubanikia samaki pamoja na mifumo ya baridi inayotumia nishati ya jua na umeme.
Kadhalima , FAO kupitia FISH4ACP imeanzisha mfumo wa kidijitali wa TANFISH MARKET unaowaunganisha wauzaji na wanunuzi wa mazao ya uvuvi kutoka maeneo mbalimbali, huku mfumo huo ukiwa na utaratibu wa malipo unaolinda fedha za pande zote mbili kwa kuhakikisha muuzaji analipwa baada ya mnunuzi kupokea mzigo.
Mtaalam wa Mnyororo wa thamani wa Uvuvi na Ufugaji wa Samaki kutoka FAO Hashimu Muumin amesema FISH4ACP ni mradi wa miaka sita unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Ujerumani na kutekelezwa na FAO, ulioanza mwaka 2020 na unatarajiwa kukamilika Desemba 31, 2026.
Amesema mradi huo unalenga kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa uvuvi, wakiwemo wavuvi, wachakataji, wasafirishaji na wauzaji wa mazao ya uvuvi, huku ukijumuisha pia shughuli za ufugaji wa viumbe maji na kilimo cha mwani.
Amesema wakati mradi huo unaanza, upotevu wa mazao ya uvuvi ulikuwa ukifikia asilimia 40 na katika msimu wa mvua uliongezeka hadi asilimia 70, hali iliyochangiwa na umbali wa maeneo ya uvuvi kutoka kwenye masoko, upungufu wa miundombinu ya kuhifadhia na kusafirisha mazao pamoja na changamoto katika mifumo ya uchakataji.
Kutokana na hali hiyo, FAO ilitoa mafunzo kwa wadau kuhusu uchakataji, ubanikaji na ukaushaji wa dagaa, sambamba na kuweka mifumo ya barafu na majokofu yanayotumia nishati ya jua na umeme.
Kwa mujibu wa Muumin hatua hizo zimepunguza kwa kiwango kikubwa uharibifu wa samaki na mazao mengine ya uvuvi, huku utafiti uliofanywa katika masoko ya ndani ukibaini kuwa asilimia 96 ya walaji wa samaki kutoka mnyororo wa Ziwa Tanganyika wanapendelea bidhaa zilizohifadhiwa katika hali ya baridi (frozen).
Kutokana na mahitaji hayo, mradi umewezesha kuwekwa kwa mitambo ya kutengeneza barafu na kuwapatia baadhi ya wachakataji majokofu yanayotumia nishati ya jua, hususan katika maeneo yasiyokuwa na umeme.
Kuhusu mfumo wa kidijitali wa TANFISH MARKET amesema unawaunganisha wauzaji na wanunuzi wa mazao ya uvuvi kutoka maeneo mbalimbali, huku mfumo huo ukiwa na utaratibu wa malipo unaolinda fedha za pande zote mbili kwa kuhakikisha muuzaji analipwa baada ya mnunuzi kupokea mzigo.
Muumin amesema mradi ulianza katika Ziwa Tanganyika na baada ya kuwafikia wadau wa Ziwa Victoria na maeneo ya Bahari ya Hindi, wameonyesha nia ya kuutumia ili kuongeza fursa za masoko.
Mradi pia umewezesha ujenzi wa Solar Tents katika vijiji zaidi ya 25 vya Ziwa Tanganyika kwa ajili ya ukaushaji bora wa dagaa, ambapo takribani asilimia 95 ya wachakataji wanaonufaika ni wanawake.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Amina Adrian Kasige, ambaye ni mvuvi na mchakataji na mmiliki wa vyombo vyabuvuvi, amesema teknolojia na elimu aliyoipata kupitia FAO imeongeza kipato chake baada ya kuacha mbinu za zamani za kukaushia dagaa kwenye mchanga, zilizokuwa zikisababisha bidhaa kukosa soko.
Amesema sasa wanauza dagaa katika masoko ya ndani na nje ya nchi, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.
Kwa kuwa FISH4ACP unakaribia kukamilika, ametoa wito kwa Serikali, taasisi, wafadhili na wadau wa maendeleo kuendeleza programu hiyo, akisema teknolojia zilizowekwa tayari zinatumika, zimeonyesha manufaa na bado kuna mahitaji makubwa ya kuendelea kuimarisha mnyororo wa thamani wa uvuvi.

