Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amezindua rasmi Mfumo wa Utabiri wa Kiasi cha Maji kwenye mito nchini, hatua inayolenga kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji.
Uzinduzi huo umefanyika kwenye Bwawa la Mindu, jijini Morogoro, ambapo Dkt. Nchimbi alikagua kwa karibu jinsi Wizara ya Maji inavyoshirikiana katika kuhifadhi, kulinda, na kukuza rasilimali hizo muhimu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Elibariki Mmasi, amefafanua kuwa mfumo huu ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Maji kupunguza changamoto zinazokabili sekta hiyo kwa kutoa taarifa sahihi na za wakati kuhusu viwango vya maji.
Amebainisha kuwa Bwawa la Mindu linatarajiwa kufaidika na mfumo huo, kwa kuwa linapokea maji kutoka sehemu mbalimbali za nchi na linachangia zaidi ya asilimia 70 ya usambazaji wa maji safi mjini Morogoro.

Aidha, sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani na kilele cha Wiki ya Maji Tanzania, Dkt. Nchimbi alipanda miti rafiki wa maji kwenye chanzo hicho, akisisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi rasilimali za maji kwa vizazi vijavyo.


