Na Lucy Ngowi
SINGIDA: JUMLA ya Sh. Bilioni 1.7 zimepatikana kutokana na harambee iliyofanywa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya CCM Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ameeleza kwamba amefanikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa kupata Sh. 1.69 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo.
Amesema kiasi hicho cha fedha ni asilimia 116 ya lengo lililokusudiwa la upatikanaji wa Sh. Bilioni 1.4.
“Nimeamua kuchukua hatua hiyo ya kuendesha harambee kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa ofisi hii, kutokana na kuchukua muda mrefu bila kukamilika ” amesema.
Wakati wa harambee hiyo, Dendego amesema jengo hilo ambalo ni la CCM lilianza kujengwa zaidi ya miaka 40 iliyopita na mzazi wake Makamu wa Rais Mteule, Emmanuel Nchimbi lakini halikukamilika ilhali likitoa viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.
“Naomba kukueleza mheshimiwa Makamu wa Rais Mteule na Katibu Mkuu wa CCM jengo la CCM Singida lilianzishwa mwaka 1985 na aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Singida wakati huo, John Nchimbi na limeendelea kujengwa kidogo kidogo lakini mpaka sasa halijaisha wala kukamilika.
“Wakati huo bado jengo hilo licha ya kutokamilika linatoa viongozi wa serikali na Chama,na sasa wewe Umekuwa Balozi na Katibu Mkuu wa Chama na hatimaye makamu wa rais Mteule kwa maana hiyo mimi na kamati yangu tuliona tuanzishe harambee kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hii ya Chama,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata amesema ujenzi wa ofisi hiyo ni muhimu kwa afya ya chama kwani likikamilika litachochea maendeleo kwa chama na kuendelea kuzalisha wana CCM kwa wingi.
Wakati wa kutangaza Matokeo ya harambee iliyochangishwa Balozi Dk.Nchimbi amesema kuwa katika kuunga mkono juhudi ya ujenzi huo Mwenyekiti wa CCM taifa ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan, amechangia Sh Milioni 50.