Na Lucy Lyatuu,Tanga
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imewahimiza wadau wa sekta ya nafaka na mazao mchanganyiko kuendelea kubuni njia bora za kusindika na kutumia mazao ya kilimo ili kuongeza thamani, kupanua fursa za masoko na kuboresha lishe kwa jamii.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyikanjijini Tanga,Ofisa Masoko Mkuu wa COPRA, Tulibako Minga, amesema mamlaka hiyo itatumia maadhimisho hayo kuonesha ubunifu mbalimbali wa usindikaji na matumizi ya mazao inayoyasimamia, kwa lengo la kuwapatia wananchi maarifa yatakayowawezesha kunufaika na mazao hayo kiuchumi na kiafya.

Minga amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu Ubunifu wako leo, lishe bora ya kesho kuelekea Dira ya mwaka 2050.
Amesema kupitia maadhimisho hayo, COPRA itaonesha mbinu mbalimbali za kuongeza thamani ya mazao, ikiwemo usindikaji wa iliki ya kijani, soya na utengenezaji wa nyama na maziwa yatokanayo na soya.
Aidha, amesema wananchi watapata fursa ya kujifunza matumizi mbalimbali ya njugu mawe katika utengenezaji wa uji, supu ya dengu pamoja na namna tofauti za kutumia mbaazi, hatua inayolenga kuhamasisha ulaji wa vyakula vyenye virutubisho na kuongeza matumizi ya mazao yanayozalishwa nchini.

Ameongeza kuwa maonesho hayo ni fursa kwa wadau wa TANGA na mikoa ya jirani kujifunza ubunifu unaoweza kusaidia kuboresha bidhaa, kuongeza ushindani katika soko na kuimarisha lishe ya kizazi kijacho.
Minga amewakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea maonesho hayo ili kujionea bidhaa na vionjo vinavyoandaliwa na COPRA, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi wananufaika kupitia maarifa, afya na matumizi bora ya mazao ya kilimo.


Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!