Na Danson Kaijage
DODOMA: MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imejikita kutoa elimu kwa wananchi na wakulima kuhusu fursa za uwekezaji katika soko la mitaji na bidhaa, kupitia maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati.
Mkurugenzi wa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa CMSA, Charles Shirima, amesema kumekuwepo na ongezeko kubwa la wawekezaji kwenye kampuni za umma na mifuko ya uwekezaji, ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“CMSA inaratibu na kusimamia uwekezaji katika hisa, hati fungani, na mifumo ya kusaidia kampuni na serikali kupata mitaji kupitia umma,” amesema Shirima.
Ameeleza kuwa wananchi sasa wanaweza kuwekeza akiba zao kwa njia endelevu kupitia mifuko ya pamoja, huku mifuko ya uwekezaji ikiongezeka kutoka mmoja hadi mingine, ikiwemo UTT-AMIS.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano na Elimu kwa Umma, Stella Anastazi, amesema CMSA pia imeanzisha soko la bidhaa ili wakulima wapate masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Naye Christopher Ngonyani kutoka CMSA amesema mfumo huo umeongeza thamani ya uwekezaji wa wananchi, huku akihimiza ushiriki zaidi wa Watanzania ambao bado hawajaanza kuwekeza.
“Tunatoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwekeza, hasa kupitia vipande ambavyo vinawapa wananchi gawio na kukuza mtaji wao,” amesema.