Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE mteule wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushindi mkubwa wa kura asilimia 97.6, akisema matokeo hayo yanaashiria imani kubwa ambayo Watanzania wanayo kwake kutokana na kazi kubwa alizozifanya katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Chatanda amesema UWT, kwa niaba ya wanawake wote nchini, inampongeza Rais Samia kwa mafanikio hayo na inaahidi kushirikiana naye katika kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, ili kuhakikisha ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi, hasa wanawake, zinatimia.

“Kama mbunge mteule wa viti maalum, nipo tayari kuisimamia utekelezaji wa ilani ya chama chetu. Tutahakikisha tunafuatilia utekelezaji wake ili wananchi, hususan wanawake, wanufaike na maendeleo yaliyopangwa,” amesema Chatanda.
Ameongeza kuwa UWT itakuwa karibu na wanawake katika ngazi zote, kusikiliza kero na changamoto zao, zikiwemo ukatili wa kijinsia na changamoto za kiuchumi, ili hatua madhubuti zichukuliwe kupitia Bunge na Serikali.
Kuhusu uwezeshaji wa wanawake, Chatanda amesisitiza kuwa Rais ameonyesha dhamira ya dhati ya kuinua uchumi wa wananchi kwa kutenga Sh. Bilioni 200 ndani ya siku 100 za kwanza za uongozi wake, kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, wakiwemo wanawake.
“Tutahakikisha wanawake wanapata mikopo ya asilimia 10 kutoka halmashauri zetu na kwamba fedha hizo zinatumika ipasavyo. Hatuishii kutoa mikopo tu; tutahakikisha akinamama wanapewa elimu na mafunzo ya matumizi bora ya fedha hizo, ili ziweze kuwanufaisha na kuwainua kiuchumi,” amesema.
Chatanda amesisitiza kuwa jukumu kubwa la UWT ni kuhakikisha kila mwanamke anapata fursa ya kujikomboa kiuchumi kupitia elimu, uwezeshaji na ufuatiliaji wa sera za maendeleo zinazogusa maisha yao.

