Na Lucy Ngowi
GEITA: WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) unashiriki katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, ambapo wanatoa huduma mbalimbali kwa wananchi na wafanyabiashara.
Kaimu Meneja wa Leseni za Viwanda kutoka BRELA, Yusuph Nakapala, amesema taasisi hiyo inatoa huduma zote muhimu za kisheria ikiwa ni pamoja na usajili wa makampuni, usajili wa majina ya biashara, alama za biashara na huduma, hataza, pamoja na leseni za biashara za Kundi A na vyeti vya usajili.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote wa mkoa wa Geita na mikoa ya jirani kufika kwenye banda la BRELA katika maonesho hayo ili kupata huduma hizo kwa urahisi.
Ametaja huduma nyingine zinazotolewa kuwa ni pamoja na uwasilishaji wa mizania ya mwaka kwa kampuni, taarifa za maendeleo ya viwanda kwa wamiliki wa viwanda, na taarifa za umiliki manufaa.

“Mwanzoni mwa maonesho mwitikio haukuwa mkubwa, lakini kadri siku zinavyoenda, wananchi wanafika kwa wingi na tunawasaidia kutatua changamoto zao.
“BRELA imeboresha mifumo yake na tunaendelea kuboresha ili huduma zipatikane kwa urahisi, siyo tu Geita bali nchi nzima,” amesema.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo, Kiliamu Simiozi, kutoka Ofisi ya Mtemi Able, amesema amefika kwa ajili ya kufanya usajili na kuongeza taarifa kwenye kampuni yao.
Ameeleza kuwa huduma zinazotolewa ni bora, lugha rafiki, na mchakato unakamilika papo hapo bila usumbufu hivyo amewahimiza ndugu na marafiki ambao bado hawajapata huduma za BRELA kufika kwenye maonesho hayo.
Naye Zedekia Gabriel, ambaye alifika kwa ajili ya kuwasilisha taarifa za umiliki’ beneficial owner’, amesema aliomba huduma hiyo muda mrefu lakini sasa amefurahi kuona ombi lake linashughulikiwa kwa haraka akiwa katika banda la Brella kwenye maonesho gayo.

Amekumbusha kuwa ni wajibu wa kila kampuni kufanikisha uwasilishaji wa taarifa kwa mujibu wa sheria.
Maonesho ya Teknolojia ya Madini ya Geita yanalenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya madini pamoja na kuwahudumia wananchi kwa karibu kupitia taasisi mbalimbali za serikali na binafsi.

