Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAFANYAKAZI wametakiwa kutimiza wajibu wao ipasavyo ili tija iwepo katika maeneo ya kazi.
Aidha waajiri wanapaswa kutimiza haki za watumishi wao kulingana na makubaliano katika mikataba yao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Joel Kaminyoge amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu TUGHE kwa mwaka 2024.

Kaminyoge amesema endapo kila upande yaani mwajiri na mfanyakazi utatimiza wajibu wake itasaidia kufanya sehemu za kazi kuwa salama, kukua kwa uzalishaji na hatimaye kufikia malengo yanayokusudiwa.
Kwa upande mwingine amesema Chama kimepiga hatua kubwa ambapo sasa kinatimiza miaka 30 tangu kilipoanzishwa.
Ametaja hatua hizo ni pamoja na huduma za ushauri wa kisheria kwa wanachama, kuimarisha mahusiano na wadau, uwekezaji katika maeneo mbalimbali ndani ya Chama pamoja na kusimamia maslahi ya watumishi nchini.


Naye Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda ameeleza kuwa Chama kinapoadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, kinajivunia kuwa mstari wa mbele katika kusikiliza kero za wafanyakazi hususani wanachama wao na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau.
Ametolea mfano migogoro inapoibuka kati ya wafanyakazi na waajiri wake TUGHE imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha suluhisho linapatikana.