Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL), imeanzisha safari za moja kwa moja za Dubai na Zanzibar, zitakazofanyika mara tatu kwa wiki, siku za Jumatano, Ijumaa na Jumapili.
Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma cha ATCL.

Taarifa hiyo inasema kutokana na kuanzishwa kwa safari hiyo, imezindua ofa ya “Safiri Zaidi, Lipa Kidogo” kwa abiria wake wanaosafiri kati ya Zanzibar na Dubai pia Dar es Salaam na Johannesburg, Afrika Kusini.
“Kupitia ofa hii, Wateja wa Air Tanzania wanaosafiri kati ya Dubai na Zanzibar au Dar es Salaam na Dubai watafaidika na punguzo la asilimia 20 a nauli lililoanza Oktoba 30, 2024,” imesema taarifa hiyo.
Imeeeza kwamba uzinduzi wa Kituo hichoi kipya cha Dubai na Zanzibar, unavutia utalii na ushindani wa biashara , pia unadhihirisha uwezo wa kampuni hiyo katika kuhudumia masoko ya kimataifa ambayo yanatoa fursa nyingi za biashara na utalii kwa wateja.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kuwajali wateja wake, abiria wa daraja la kawaida wameongezewa idadi ya mabegi hadi kufikia matatu yenye uzito usiozidi kilo 23 kwa kila begi na mabegi manne kwa daraja la biashara, kuanzia Oktoba 30, mwaka huu.
Katika hatua nyingine kampuni hiyo imerejesha safari zake za Johannesburg nao pia watanufaika na ofa “Safiri Zaidi, Lipa Kidogo” wakiwa kwenye ndege mpya za kisasa B737-9 Max kwa hadhi sawa na safari za kimataifa.