Na Mwandishi Wetu
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema maendeleo ya kudumu hayawezi kupatikana bila amani, na kwamba amani ya kudumu haiwezi kupatikana bila maendeleo jumuishi na endelevu.
Amesema hayo kutokana na kauli mbiu ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika jijini Kinshasa Novemba 15, 2025, isemayo: ‘Kuimarisha Amani na Usalama kwa ajili ya Maendeleo Endelevu kwenye Eneo la Maziwa Makuu.’.

Dkt. Nchimbi amesema eneo la Maziwa Makuu limebarikiwa na utajiri mkubwa wa maliasili, zikiwemo madini adimu na rasilimali watu, lakini bado linakabiliwa na migogoro ya kisiasa ya muda mrefu inayochochewa na masuala mbalimbali kama uvunaji haramu wa maliasili.
Amesema migogoro hiyo imesababisha majanga ya kibinadamu, ikiwemo watu kukimbia makazi yao na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaotokana kwa kiasi kikubwa na uhalifu wa kivita.
Ameeleza kuwa sambamba na jitihada za kikanda na kimataifa zinazoendelea kudhibiti migogoro hiyo, Tanzania kama nchi muasisi wa ICGLR imehusika katika jitihada mbalimbali za kukomesha migogoro ndani ya kanda, ikiwemo kuchangia vikosi vya kulinda amani nchini DRC na kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi za SADC na EAC uliolenga kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa Mashariki mwa DRC.

Makamu wa Rais amepongeza jitihada mbalimbali zinazoendelea katika kutafuta ufumbuzi wa migogoro katika nchi za ICGLR.
Jitihada hizo ni pamoja na zinazongozwa na Rais wa Angola, João Lourenço, za kutafuta amani nchini DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati; kusainiwa kwa mkataba wa amani nchini Qatar; kuunganishwa kwa michakato ya Luanda na Nairobi; na mkataba wa amani kati ya Rwanda na DRC uliosainiwa chini ya usimamizi wa Serikali ya Marekani.
Nchimbi amesema licha ya jitihada hizo, bado kuna changamoto za kiusalama katika nchi mbalimbali, hususan DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Sudan.
Amehitimisha kwa kusema kuwa njia ya kuelekea amani inahitaji ushirikiano na dhamira ya dhati kutoka nchi zote za ICGLR ili kukabili changamoto zilizosalia kwa ajili ya kujenga ukanda wenye amani, ustawi na himilivu kiuchumi.

