Na Lucy Ngowi
MBEYA: WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kuacha kuwaficha vijana wenye ulemavu na badala yake wawape fursa ya kupata mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Baraka Shekimweri ametoa wito huo alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mkoani Mbeya.
“Nimefurahishwa kuona vijana wengi wenye ulemavu wakiwa mafundi cherehani, wataalamu wa TEHAMA, na wabunifu wa kazi mbalimbali. Huu ni ushahidi kuwa ulemavu si kikwazo cha mafanikio,” amesema.
Shekimweri ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Elimu kutoka Makao Makuu ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi na Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari, Ufundi Stadi na Utafiti (RAAWU), ameongeza ni muhimu jamii kuacha kuwahifadhi vijana hao majumbani kwa dhana kuwa hawawezi kufanya lolote,
Kwani wameonyesha uwezo mkubwa wa kujifunza na kufanya kazi za kitaalamu kwa ustadi.
Shekimweri amesema, “Huu ni wakati wa kuwekeza kwa vijana wetu kwa kuwapatia ujuzi wa kiufundi ambao utawawezesha kujiajiri na kuondokana na utegemezi.”