Na Mwandishi Wetu
GEITA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ametembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Maonesho ya Nane ya Madini yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoani Geita.
Akiwa kwenye banda hilo ameipongeza NSSF kwa huduma zake za kidijitali kwa wananchi na wadau.

Waziri Mkuu Majaliwa akiwa kwenye banda hilo Septemba 22, mwaka huu 2025, amepokea maelezo kutoka kwa Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Masha Mshomba, kuhusu jitihada za Mfuko kutekeleza maelekezo ya Serikali ikiwemo kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inaendelea kutolewa kwa sekta binafsi na wananchi waliojiajiri.
Lulu amesema: “Mafanikio yetu makubwa yametokana na mwongozo wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, rahisi na kwa wakati kupitia mifumo ya kidijitali.”

Pia amemwonesha Waziri Mkuu mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma zote kwa mwanachama, ikiwemo huduma zinazopatikana kupitia simu za kiganjani, iwe ni simu janja au ya kawaida, ambapo wote wanahudumiwa na NSSF kidijitali.
“Wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, thamani ya Mfuko ilikuwa Sh.i Trilioni 4.8, na sasa imefikia Trilioni 9.9,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Geita, Winniel Lusingu, amewataka wananchi kutembelea banda la NSSF ili kupata elimu ya hifadhi ya jamii.