Na Lucy Lyatuu
MRADI wa Thamini Uzazi Salama unaolenga kupunguza vifo vya mama na Watoto wachanga nchini umekabidhiwa vitendea kazi mbalimbali, mavazi ya kujikinga kwa wahudumu wa afya ya jamii 56 pamoja na magari mawili.
Mradi huo wa miaka saba wa kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya katika jamii unatekelezwa na Chama cha wakunga Tanzania (TAMA) kwa kusimamiwa na Shirika la Umoja Wa Mataifa Linaloshughulikia Masuala Ya Afya Ya Uzazi Na Idadi Ya Watu Duniani (UNFPA), Chama Cha Wakunga Canada (CAM), Amref Health African na Wizara ya Afya.
Mradi huo unalenga wilaya tatu mkoani Shinyanga na Halmashauri tatu za Dares Salaam.
Akizungumza katika makabidhiano ya vifaa hivyo Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa mkoa, Albert Chalamila, Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema serikali inatambua mchango wa wadau wa maendeleo katika kuhakikisha afya za wananchi zinaimarika.
Amesema serikali inatambua mchango na kazi kubwa inayofanywa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika kufuatili hali za kina mama wajawazito, kutoa elimu ya afya, kutoa rufaa na pia kukusanya taarifa muhimu za kiafya.
“ Ili waweze kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi wanahitaji mazingira bora ya kazi ikiwemo upatikanaji wa vifaa stahiki,” amesema na kuongeza kuwa wanakabidhi baiskeli, makoti ya mvua, Mabuti ya mvua Pamoja namabegi yakubebea vitendea kazi mbalimbali.
Amesema vifaa hivyo vitaongeza ufanisi wa kazi ili kutimiza lengo la mradi huo wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kina mama na Watoto wachanga.
Amesema mradi umewezeshwa kwa ufadhili wadola milioni 11.75 za Canada kutoka serikali ya Canada na tayari umeonesha mafanikio ikiwemo kuboresha mafunzoya wakunga, kuwawezesha wahudumu wa afya ya jamii na kupunguza vifo vya kina mama na Watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini Tanzania Mark Schreiner amesema ni hatua muhimu inayoonesha mafanikio ya uwekezaji wa watu ambapo wanajenga mfumo wa afya thabiti ambapo kila uzazi ni salama na kila mama anapata huduma bora na yenye heshima.
Amesema chini ya mradi huo wakunga sasa wana mafunzo bora na msaada wa kitaalam, jamii zina uelewa zaidi, mila kandamizi zinapigwa vita na wanaume wakishiriki katika afya yauzazi.
Rais wa TAMA, Dk Beatrice Mwalike amesema kupitia mradi huo wakunga 180 wamefundishwa kutoa huduma za dharura kwa wamama wajawazito na Watoto wachanga 90 mkoa wa Dares Salaam na 90 Shinyanga.
Aidha vituo mbalimbali vimefikiwa ikiwemo hospitali nane kwa mkoa wa Dares Salaam, vituo vya afya 24 na zahanati 27 a kufikisha jumla ya vituo 59. Kwa mkoa wa Shinyanga jumla ya hospitali nne, vituo vya afya 22 na zahanati 46 jumla ikiwa ni vituo 72.