KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki kikao cha awali cha Maofisa Waandamizi cha Jukwaa la Majadiliano kati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Serikali ya Marekani kilichofanyika Antananarivo, Madagascar, leo Agosti 13, mwaka huu 2025.
Akifungua majadiliano hayo, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda, Angeles N’Tumba, amesema kikao hicho, ambacho ni cha kwanza kufanyika, kitajadili miongozo ambayo SADC na Marekani wataitumia katika ushirikiano wao,
Ambao umelenga maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na amani na usalama, afya, uchumi, na usimamizi wa rasilimali kama vile nishati na madini.
Mwakilishi wa Serikali ya Marekani, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Melanie Higgins, ameihakikishia SADC kuwa, licha ya mabadiliko ya sera katika Serikali ya Marekani, nchi hiyo imedhamiria kwa dhati kushirikiana na SADC, na ndiyo maana yeye na ujumbe wake wametumwa kushiriki kikao hicho.
Amesema kuwa Marekani ipo tayari kushirikiana na SADC kutatua changamoto zinazoikabili kanda hiyo, hususan zile zinazorejesha nyuma utekelezaji wa miradi ya maendeleo, amani na usalama.
Inaelezwa kuwa jukwaa hilo la majadiliano ni kielelezo cha dhamira ya dhati na ya pamoja kati ya SADC na Marekani katika kukuza na kuimarisha ushirikiano endelevu, mtangamano wa kikanda, na kuibua fursa za kiuchumi kwa manufaa ya pande zote.