Asisitiza Kuendeleza Safari ya Tumaini kwa Walimu
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: RAIS wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwalimu Suleiman Ikomba, ameeleza kusononeshwa na baadhi ya Maofisa wa Halmashauri kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi, licha ya serikali kuu kutoa maelekezo ya wazi juu ya maslahi ya walimu.
Ameeleza hayo alipozungumza na Mwandishi wa habari hii alipotaka kujua ni nini kinachomsononesha kuhusu waalimu hapa nchini.
Amesema moja ya mambo yaliyomvunjia moyo katika safari yake ya uongozi ni kukutana na walimu waliopaswa kupandishwa madaraja kwa mujibu wa sifa zao, lakini wakaachwa kwa sababu ya uzembe wa maofisa wa utumishi katika ngazi ya halmashauri.
“Tumeona walimu waliokuwa na sifa sawa, waliopaswa kupanda madaraja pamoja, lakini mmoja anapandishwa na mwingine anaachwa.
“Wengine wanazidiwa mshahara kwa zaidi ya laki mbili ilhali wameajiriwa siku moja, wana elimu sawa, na wanatekeleza majukumu sawa. Hali hii ni ya kusikitisha na inawaumiza walimu,” amesema.
Amesema uzembe huo unaofanywa na baadhi ya maofisa ni chanzo kikuu cha malalamiko yasiyopaswa kuwepo, hasa ikizingatiwa kuwa serikali kuu imeonyesha nia thabiti ya kutatua changamoto za walimu kupitia maagizo rasmi yanayopaswa kufanyiwa kazi kwenye halmashauri.
“Maagizo kutoka serikali kuu yalikuwa wazi. Tukiwa pamoja na viongozi wa serikali tulitembelea mkoa kwa mkoa, tukakutana na walimu, tukapokea malalamiko yao. Cha kusikitisha ni kuona baadhi ya halmashauri wakishindwa kutekeleza maagizo hayo. Huu ni uzembe wa mtu mmoja lakini unagharimu maisha ya wengi,” amesema.
Kwa upande mwingine ameelezea kufurahishwa na namna ambayo serikali imekuwa ikishirikiana na CWT katika kuzishughulikia kero za walimu.
“Jambo lililonipa furaha isiyoelezeka ni namna tulivyotembea na serikali mkoa kwa mkoa kupitia kliniki ya walimu, tukisikiliza kero zao, tukitafuta suluhu. Kupokelewa na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, walimu wakifunguka matatizo yao moja kwa moja hiyo ilikuwa safari ya matumaini,” amesema.
Ameahidi katika kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano kutoka mwaka huu 2025 hadi 2030, kwamba atahakikisha CWT inabaki kuwa sauti ya kweli ya walimu wote.
Amesema anataka kuwa kiongozi mtetezi wa haki katika kiwango cha ubora unaostahili.
“Natamani kuwa mtetezi wa walimu, lakini kwa njia inayolinda hadhi ya taaluma yetu. Nimegombea kwa sababu nimeona kuwa kazi nzuri imeanza kufanyika.
“Niko hapa kuwahudumia kwa ukamilifu, na kuhakikisha kazi yetu ya ualimu inabaki kuwa yenye heshima na tija kwa taifa,” amesema.