– Mwenyekiti Mlimuka Atembelea Banda la Sabasaba
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Tume ya Ushindani (FCC), Dkt. Aggrey Mlimuka, ameipongeza tume hiyo kwa juhudi madhubuti inazochukua katika kudhibiti bidhaa bandia na kukuza ushindani wa haki sokoni.
Amesema mafanikio hayo ni sehemu ya jitihada za serikali kulinda walaji na kuimarisha mazingira ya biashara nchini.

Dkt. Mlimuka alitoa pongezi hizo alipotembelea Maonesho ya 49 ya Kibiashara yajulikanayo kama Sabasaba mkoani Dar es Salaam alipotembelea banda la Tume ya Ushindani (FCC).
Banda hilo liko ndani ya eneo la Wizara ya Viwanda na Biashara, mkabala na banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Akizungumza na wafanyakazi wa FCC waliopo kwenye banda hilo, Dkt. Mlimuka amesisitiza umuhimu wa tume hiyo kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya bidhaa bandia na umuhimu wa ushindani wa haki katika ukuaji wa uchumi.
“Tume imekuwa ikifanya kazi nzuri kwa kuhakikisha kwamba bidhaa bandia zinadhibitiwa na ushindani wa haki unalindwa. Hii ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda vyetu na ustawi wa mlaji wa kawaida,” amesema.
Amesema Maonesho ya Sabasaba ni jukwaa muhimu kwa taasisi kama FCC kuelimisha wananchi kuhusu majukumu yake na kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha soko huru na lenye uwiano wa ushindani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa FCC, Roberta Feruz, amesema ushiriki wa FCC katika maonesho hayo unaendelea kuleta mafanikio makubwa katika kuelimisha umma kuhusu haki zao kama walaji na wajibu wao katika kusaidia kudhibiti bidhaa haramu sokoni.

“Tumekuwa tukipokea wananchi wengi wanaokuja kutaka kufahamu namna ya kutambua bidhaa bandia, haki zao wanaponunua bidhaa, na namna ya kutoa taarifa iwapo wana mashaka na bidhaa fulani. Hili linaonyesha mwamko mzuri,” amesema.