Na Lucy Lyatuu
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imesema imefanikiwa kulipa jumla ya Sh bilioni 9.07 hadi kufikia Machi 2025 kwa wateja waliokuwa na amana katika benki saba zilizofungwa kutokana na kufilisika.
Hata hivyo imewataka wananchi kutembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika maonyesho ya Sabasaba ili kupata elimu zaidi kuhusu jinsi wanavyolindwa na mfumo huo wa bima endapo taasisi za kifedha zitakumbwa na matatizo.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea Dar es Salaam Mkurugenzi wa DIB Isack Kihwili amesema kiwango hicho cha malipo kimegusa wastani wa asilimia 75.76 ya jumla ya fidia zote zinazostahili kulipwa.
Alizitaja benki zilizohusika kuwa ni pamoja na FBME ambayo zaidi ya asilimia 57 ya fidia zake tayari imelipwa, Covenant Bank asilimia 83.73, Kagera Farmers’ Cooperative Bank asilimia 94.06, Meru Community Bank asilimia 92.35, Mbinga Community Bank asilimia 84.66, Njombe Community Bank asilimia 87.26 na Efatha Bank ambayo bado inaendelea kufanyiwa tathmini ya fidia.
Amesema wateja ambao bado hawajalipwa ni wale tu ambao hawajawasilisha madai yao ambapo tunawashauri kuwasilisha nyaraka zao ili waweze kulipwa stahiki zao.
Amesema Bodi hiyo ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1991 na kuanza kazi mwaka 1994 ikiwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sasa inajiendesha yenyewe kwa mafanikio.
Amesema hadi kufikia Desemba 2024, bodi ilikuwa na mtaji wa sh trilioni 1.3, ikiwa ni matokeo ya kuongezeka kwa taasisi za fedha zinazochangia pamoja na maboresho ya mifumo ya usimamizi.

Amesema Kwa sasa kuna jumla ya wachangiaji 42 ambao ni mabenki yaliyosajiliwa na BoT, na huchangia asilimia 0.15 ya amana kwa mwaka kama michango ya bima.
Ameongeza kuwa kiwango cha juu cha fidia kwa mteja mmoja kilikuwa sh 250,000 lakini kikaongezeka hadi sh milioni 1.5 kwa mwaka 2010, na kufikia sh milioni 7.5 tangu mwaka 2023.
“Kiasi hiki kinamaanisha kuwa, kwa benki yoyote itakayofungwa kwa sasa, mteja mwenye amana ya shilingi milioni saba na nusu au chini ya hapo atalipwa fidia kamili mara moja,” amesema na kuongeza kuwa iwapo mteja ana zaidi ya kiwango hicho basi Bodi itafuata taratibu nyingine za usimamizi wa mali za benki hiyo kwa mujibu wa sheria za ufilisi,” amesema.
Ameongeza kuwa Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 99.24 ya wateja wa benki zote nchini wamekingwa na mfumo huo wa bima ya amana, kiwango ambacho kiko juu ya kiwango cha kimataifa kinachotakiwa cha asilimia 90.
Aidha amesema zipo changamoto kwa wateja wa benki zilizo na matawi au ushirikiano na taasisi kutoka nje ya nchi kutokana na utofauti wa mifumo ya kisheria na kifedha.
Kihwili aliwataka wananchi kutembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika maonyesho ya Sabasaba ili kupata elimu zaidi kuhusu jinsi wanavyolindwa na mfumo huu wa bima endapo taasisi za kifedha zitakumbwa na matatizo.