Na Lucy Lyatuu
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limesema kupitia msimu wa Maonesho Ya 49 Ya Kimataifa Ya Biashara maarufu kama sabasaba limeweka punguzo kubwa kwenye vifaa vya simu (mobile ) ambavyo ni Router, USB modem, na MIFI Ili kuwawezesha wateja kumiliki vifaa hivyo na kufurahia ulimwengu wa kidigitali katika kurahisisha mawasiliano.
Aidha shirika hilo limeijipambanua kama muunganishaji thabiti Wa mawasiliano likizingatia na usalama wa huduma za kwa wateja.
Akizungumza katika Maonesho hayo yanayoendelea Dar es Salam Meneja wa Banda la TTCL, Janeth Maeda, ametoa wito kwa Watanzania kutembelea banda la TTCL ili kujionea huduma za kibunifu, zinazojibu mahitaji halisi ya sasa ya Taasisi, Mashirika na wananchi wa kawaida.

Maeda amesema Shirika hilo linatumia Maonesho hayo kuuhabarisha umma namna linavyotekeleza wajibu wake kwa Wananchi likiwa limeaminiwa na serikali na kupewa dhamana ya kusimamia na kuendesha miundombinu ya kimkakati ya serikali ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).
“TTCL ni suluhisho la sasa na la baadaye katika huduma za TEHAMA. Hii ndiyo sababu Serikali imeendelea kutuamini kusimamia miundombinu ya kitaifa yenye umuhimu mkubwa kwa usalama wa Taifa na maendeleo endelevu ya kiuchumi,” amesema Maeda.
Amesema TTCL inatoa huduma kwa Taasisi nyingi za Umma ambazo zimeonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Amezitaja taasisi hizo ni pamoja na taasisi za Kifedha, Wizara zote, Taasisi na Mashirika ya kiserikali, Sekta ya madini, sekta zisizo za kiserikali, sekta ya Afya na elimu, sekta ya usafirishaji pamoja na sekta ya utalii.
Maeda ameongeza kuwa kwa kutumia huduma za TTCL kupitia Mkongo wa Taifa, Mawasiliano, huduma za Kuhifadhi Data Kimtandao ndani ya nchi, na usambazaji wa mifumo ya TEHAMA, taasisi hizo zimepiga hatua kubwa katika kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za mawasiliano na kuimarisha usalama wa taarifa zao.
“Kupitia teknolojia yetu ya fiber optic, tumeweza kuwahudumia mashirika haya kwa kasi ya kuaminika, jambo ambalo linaongeza tija na usalama katika utendaji wao wa kila siku,” ameongeza Maeda.

Amewaalika washiriki wa Maonesho Kujionea teknolojia ya mawasiliano ya kisasa inayowezeshwa na mtandao wa TTCL, kujifunza kuhusu namna bora ya kidigitali ya uhifadhi salama wa taarifa (Data Center), na kupata maarifa ya namna ya kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.