Na Danson Kaijage
DODOMA: JESHI la polisi Mkoa wa Dodoma limewaomba wakazi wa Mkoa huo kutoa taarifa za watu wanaowadhania wanaweza kuwa na viashiria vya uhalifu ili watiwe nguvuni.
Ombi hilo limetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari juu ya taarifa ya kukamatwa watu ambao wanadhaniwa ni waharifu katika maeneo mbalimbali katika Mkoa huo.
Katabazi amesema jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wanne kwa kosa la kupatikana na silaha bila kuwa na kibali katika wilaya za Dodoma mjini na Mpwapwa.
Amesema Mei 17, mwaka huu 2025 majira ya saa kumi kamili jioni katika mtaa wa kikuyu mission jijini Dodoma walikamatwa watuhumiwa wawili wote wakazi wa kikuyu mission wakiwa na bastora ikiwa na risasi 13 kwenye magazine yake.
Kamanda huyo amesema.Mei 19 mwaka huu majira ya saa 11: 00 jioni katika mtaa wa Lukole wilaya ya Mpwapwa walikamatwa watuhumiwa wegine wawili wakiwa na silaha iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za Shortgun iliyokatwa mtutu na kitako pamoja na risasi tano.
Aidha Mei 18 mwaka huu, saa n 4: 40 usiku, mtaa wa Mbuyuni Kata ya Kizota walikamatwa Nestory Kimario (38) na Thomas Paschal maarufu kwa jina la Sigan (28), wote wakazi wa Mbabala.
Amesema watuhumiwa hao wamekutwa na mafuta aina ya Dizeli lita 2420 yakiwa kwenye madumu 89 yaliyohifadhiwa kwenye gari aina ya Toyota yenye namba za usajili T273BKB.
Kamanda Katabazi amesema katika msako wamekamata vifaa mbalimbali vya kuvunjia, TV sita na redio saba ,ambazo zinadaiwa kuwa mali za wizi.