Na. Mwandishi Wetu
UBORESHAJI wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili utafanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kuanzia Mei Mosi, 2025 na kukamilika Julai nne, 2025.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele hayo leo alipozungumza na Waandishi wa Habari.
Amesema uboreshaji wa Daftari utafanyika kwa mizunguko mitatu ambapo mzunguko wa kwanza utajumuisha mikoa 15, mzunguko wa pili mikao 16 na mzunguko wa tatu utajumuisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo.
Ameitaja mikoa itakayohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kuwa ni Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo kazi hiyo itafanyika Mei mosi hadi saba, 2025.
Mikoa ya mzunguko wa pili ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo kazi hiyo itafanyika Mei 16 hadi 22, 2025.
“Mzunguko wa tatu wa kazi hiyo utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Juni 28, 2025 hadi Julai nne, 2025,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema uboreshaji huo kwa awamu ya pili, utafanyika ngazi ya Kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya Jimbo kwa Tanzania Zanzibar, ambapo jumla ya vituo 7,869 vitahusika, vituo 7,659 vipo Tanzania Bara na vituo 210 vipo Tanzania Zanzibar.
“Tunatarajia kuwa katika awamu ya pili ya uboreshaji, wapiga kura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari,” amesema.
Amesema uandikishaji huo utahusisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine.
Pia amesema lengo la uwekaji wazi wa Daftari hilo ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa.
Tume iliboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza kuanzia tarehe Julai 20, 2024 na kukamilisha Machi 25, 2025.