Na Mwandishi Wetu
SONGWE: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi , Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amezindua miradi yenye thamani ya Sh. Bilioni 1.6 ya elimu, umeme na barabara katika Halmashauri ya wilaya ya Songwe mkoani Songwe
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo, amesema mradi wa Ujenzi wa shule ya Maweni B uliogharimu Sh. Milioni 583 utasaidia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kwa watoto wa Mkwajuni, kupunguza msongamano darasani pamoja na utoro wa rejareja.

Ridhiwani pia amezindua madarasa Sita yatakayotumika kwa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Kanga.
Mradi huo wenye thamani ya Sh. Milioni 150 utawezesha vijana kuishi bweni na kuboresha mazingira ya malazi na Ujifunzaji kwa wanafunzi.
Vile vile amezindua ujenzi wa barabara za Mkwajuni mjini kwa kiwango cha lami wenye thamani ya Sh. Milioni 760.
Kwa upande mwingine amempongeza Mbunge wa jimbo la Songwe, Philipo Mulugo kwa kuelekeza kiasi cha Sn.Milioni 500 za mfuko wa maendeleo ya Jimbo kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Katika hatua nyingine, Kikwete amezindua Mradi wa usambazaji umeme Kitongoji cha Kikuyuni kata ya Mkwajuni wenye thamani ya Sh. milioni 156.
Amesema, fedha hizo zimetolewa na serikali kwa lengo la kuchochea maendeleo na ustawi wa watanzania hususani waishio vijijini.
Mkuu wa mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amemhakikishia.Waziri huyo kuendelea kutekeleza miradi kwa ufanisi ili kuweza kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi za wananchi wa mkoa huo.
Vile vile Chongolo amewahimiza wananchi kulinda na kuyatetea maendeleo yao kwa wivu kwa kuwa hilo ndilo lengo la Serikali yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mara baada ya kuzindua miradi hiyo, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kuridhishwa na kasi ya maendeleo.