Na Mwandishi Wetu
GEITA: RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amewataka wanachama wa CCM kuweka mbele maslahi ya chama, pamoja na kudumisha umoja na mshikamano.
Kikwete amezungumza hayo alipohutubia katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika katika Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita.
“Wekeni mbele maslahi ya Chama chetu, watajitokeza watu mbalimbali kuja kugombea nafasi mbalimbali wapokeeni lakini wakitokea wenye maneno tu waambieni sie tunataka maendeleo sio maneno,” amesema Kikwete.
Pia ameupongeza uongozi wa CCM Wilaya ya Bukombe kwa Mkutano Mkuu Maalum wa kutoa taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM Jimbo la Bukombe kwa mwaka 2020-2025.
“ Nawapongeza kwa kuandaa Mkutano huu kwa kuwa unakidhi takwa la katiba ya CCM kwa kuwa inawezesha kupima mlipotoka, mlipo na mnapokwenda.

“Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 1977 toleo la 2022 katika Ibara ya 72 (1) inatambua kuwa Mkutano Mkuu ni kikao kikubwa cha Chama katika ngazi ya wilaya, aidha Ibara ya 74 imetamka kazi za msingi za Mkutano huu kuwa ni kuzungumza mambo yote yanayohusu ulinzi na usalama na maendeleo kwa ujumla katika wilaya,” amesema.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM Bukombe amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi zilizosaidia utekelezaji wa idadi kubwa ya miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo.
“Nyie wenyewe mmeona yaliyofanyika Bukombe ni mengi sana na hakuna mkoa wilaya au jimbo ambalo halikuguswa na Rais Samia.
“Hii ndio sababu ya msingi iliyofanya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika Dodoma Januari mwaka huu kumchagua kuwa mgombea wa chama chetu kwa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” amesema.

Pia amewaambia wana Jimbo kuwa hawakufanya makosa kumpa kura Dotto Biteko kwa kuwa mambo mazuri yasingetokea kama wasingemchagua.
Kikwete amewataka wananchi wa Bukombe kuwachagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kuendeleza miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo.
Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Doto Biteko amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.
“ Nianze kwa kusema kwa yote yaliyotekelezwa katika Jimbo hili yametokea kwa sababu ya matashi mema ya Rais Samia Suluhu Hassan, anatupenda sana wananchi wa Bukombe, kwa kipindi ambacho nimekuwa mbunge nimeona ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Jimbo leo,” amesema.
Vilevile, amesema Rais Samia ameridhia ujenzi wa barabara ya kutoka Ushirombo hadi Katoro kwa kiwango cha lami na kuwa mkandarasi anatafutwa kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amempongeza Kikwete kwa jitihada alizofanya wakati wa uongozi wake kwa kujenga msingi mzuri wa kuhakikisha watoto wanapata elimu nchini.