Na Mwandishi Wetu
DODOMA: KAMATI ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeridhishwa na utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake, jinsi inavyowagusa wananchi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq, ameelezea kuridhishwa huko, wakati kamati hiyo ilipopokea taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024.
Fatuma amesema kamati hiyo pia imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kukuza ustawi na maendeleo ya Watanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amesema ofisi hiyo katika mwaka wa fedha 2024/2025 imepanga kuendelea kutekeleza shughuli mbalimbali.
Ametaja shughuli hizo ni pamoja na usimamizi wa kazi na huduma za ukaguzi, maendeleo ya vijana, kuratibu shughuli za ajira, utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu, hifadhi ya jamii, na ukuzaji wa tija.

Ridhiwani ameahidi kuwa ofisi hiyo itatekeleza majukumu hayo kikamilifu ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.