Na Mwandishi Wetu
ARUSHA:WAZIRI wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amefungua mafunzo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), yanayohusu Usimamizi wa Fedha za Umma.
Mafunzo hayo yameandaliwa na wizara hiyo kupitia Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).
Akifungua mafunzo hayo, Nchemba ameipongeza kamati hiyo kwa kutekeleza kikamilifu jukumu lake la msingi la usimamizi wa fedha za umma na kukuza utawala bora katika nchi hatua ambayo imeisaidia serikali kuboresha maandalizi ya hesabu za Serikali, kuimarisha mifumo ya kielekroniki ya usimamizi wa fedha za umma, na kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa bajeti inayoidhinishwa na Bunge.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya PAC, Josephat Hasunga ameishukuru wizara hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wajumbe wa kamati hiyo, kwa kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi wa kuelewa namna Serikali kupitia Wizara ya Fedha inavyotekeleza majukumu yake kikamilifu katika usimamizi wa Fedha za umma zinazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya jamii na kukuza uchumi wa nchi.