Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM:WANANCHI wanapaswa kuelimishwa na kuelewa sera, sheria, mifumo, kanuni na miongozo inayosimamia matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa ili kuondoa hofu na dhana potofu kuhusu teknolojia hiyo miongoni mwa baadhi ya watu.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Toba Nguvila amesema hayo katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Bioteknolojia Tanzania (BST),alipomwakilisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa RAIS, Cyprian Luhemeja.
Nguvila amesema utoaji elimu huo ni jukumu la kila mmoja ikiwemo serikali na asasi mbalimbali ikiwemo BST.
‘’Ninaamini kuwa ushirikiano miongoni mwetu ni moja ya nyenzo muhimu katika kufanikisha matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa kwa maendeleo ya nchi yetu.
‘’Kwa hiyo tunatarajia kupata ushirikiano timilifu na endelevu kutoka kwenu katika kuelimisha wananchi dhana nzima ya bioteknolojia kwa kukuza uelewa kwa jamii kuhusu faida za bioteknolojia hasa katika sekta ya kilimo,”amesema.
Amesema anaelewa kwamba BST kimekuwa kinaendesha semina na mashauriano mbalimbali ya kukuza uelewa na ufahamu wa wadau wengine kwa kuchangia katika kukuza uelewa wa jamii kuhusu teknolojia hiyo.
Amewataja wadau hao kuwa ni pamoja Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, vyuo vikuu, vituo vya utafiti nchini, vyombo mbalimbali vya habari, program ya Jukwaa la Biotekinolojia (OFAB)Tanzania na Shirika la Kimataifa linalohusika na Biotknolojia ya Kilimo kwa kujihusisha na uhandisi wa vinasaba (ISAAA)
Pia amesema pamoja na vyuo kujenga uwezo wa rasilimali watu wa kuendeleza tasnia ya bioteknolojia, wahitimu wa kozi hiyo wanakosa ajira hivyo amelichukua kwa ajili ya kulifikisha wizara husika ili liweze kupatiwa ufumbuzi.
Amesema itakuwa haina maana yoyote kwa vyuo kuendeleza kuzalisha wataalam wa tasnia hiyo muhimu halafu wanashindwa kuingia katika soko la ajira.
Naye Mwenyekiti wa BST, Profesa Peter Msolla amesema kwa mwaka 2024 taasisi hiyo imeendelea kuchangia utekelezaji wa sera ya Mazingira ya mwaka 2021 iliyozinduliwa na Makamu wa Rais Philip Mpango Februari 12, 2022.
‘’Asasi yetu inazingatia maelekezo ya kisera yanayolenga, pamoja na mambo mengine katika uhifahi wa mazingira, kujenga uwezo na uelewa katika usimamizi na matumizi salama ya biotknolojia ya kisasa,’’amesema.
Amesema serikali imejikita katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo ya watu kwa kurejea dira ya Maendeleo ya watu kwa kurejea dira ya taifa na kuandaa muendelezo wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.